Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) limetangaza kuipoka Simba pointi
tatu na mabao matatu ambazo ilipewa kutokana na mchezo wao dhidi ya
Kagera Sugar.
Wiki mbili zilizopita Simba ilipoteza mchezo dhidi ya Kagera kwa
kufungwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera katika Ligi
Kuu ya Bara lakini baadaye ilikata rufaa ikipinga Kagera kumtumia
mchezaji Mohamed Fakhi ikidai alikuwa na kadi tatu za njano, ndipo
ikapewa ushindi huo kupitia Kamati ya Saa 72.
Maamuuzi haya yanakuja baada Kagera Sugar kuomba kufanya marejeo ya
hukumu yao ya kupokwa pointi tatu na kamati ya saa 72 kwa madai ya
kumchezesha Mohamed Fakhi mwenye kadi tatu za njano, ndio Katibu wa TFF
akaitisha kikao cha kamati ya katiba, sheria na hadhi za wachezaji
kupitia marejeo (review) ya hukumu hiyo.
KAMATI ya Katiba, Sheria na Hadhi za wachezaji imetengua maamuzi ya
kamati ya Usimamizi na mashindano (kamati ya saa 72) kwa kuipoka Simba
pointi tatu na mabao walizopewa na kamati ya saa 72 kwa madai ya
kumchezesha Mohamed Fakhi mwenye kadi tatu za njano.
Akizungumza na waandishi wa habari juu ya uamuzi huo, Katibu Mkuu wa
TFF, Selestine Mwesigwa amesema kuwa kuna sababu kadhaa zimechangia
kuchukuliwa kwa maamuzi hayo ambapo alizitaja kuwa ni:
“Malalamiko ya Simba hayakuwasilishwa kwa wakati muafaka tangu mchezo
ulipochezwa, malalamiko yao hayakuwa katika njia ya maandishi, rufaa ya
Simba haikulipiwa ada, kikao cha Kamati ya Saa 72 kilikosa uhalali
kutokana na kuwashirikisha watu ambao hawana uhalali wa kuwa kwenye
kikao.
“Kutokana na sababu hizo kamati imeamua kutengua maamuzi yaliyochukuliwa
na Kamati ya Saa 72 na kurejesha matokeo kama yalivyokuwa, pia kamati
imemuagiza katibu mkuu wa TFF kuwapeleka baadhi ya wajumbe wa bodi ya
ligi katika Kamati ya Maadili ya TFF kwa kosa la kwenda kinyume na kazi
zao,” alisema Mwesigwa.
Pia Mwesigwa amesema maamuzi yaliyofikiwa na kamati ya katiba, Sheria
na hadhi za wachezaji ni ya Mwisho hayakatiwi rufaa sehemu yoyote.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni